Jumanne , 26th Mei , 2020

Chama cha CHADEMA kupitia kwa Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa chama hicho, Tumaini Makene, kimesema kuwa mpaka sasa hivi hakuna tangazo lililotoka ambalo, linawapa nafasi watangaza nia za kugombea Urais ndani ya chama hicho, kuwasilisha taarifa zao kwa Katibu Mkuu wa chama hicho.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa CHADEMA, Tumaini Makene

Makene ameyabainisha hayo leo Mei 26, 2020, wakati akizungumza kwenye kipindi cha SupaBreakfast ya East Africa Radio na kuongeza kuwa kwa mwanachama yeyote wa chama hicho, hata kabla ya kutangaza nia ya kugombea ni lazima atakuwa ameisoma na kuilewa katiba ya CHADEMA.

"Lakini kabla ya kuwasilisha, katika sehemu ambayo unakuwepo kunakuwa na tangazo limetoka na watu wanapeleka makusudio yao ofisi ya Katibu Mkuu, halafu process zingine zinafuata kwa mujibu wa chama, na tangazo la watu kuwasilisha nia zao bado halijatoka" amesema Tumaini Makene.

Aidha Makene ameongeza kuwa,"Tunaamini kwamba kwa mtu yeyote ambaye ni mwana CHADEMA, anafahamu utaratibu kabla ya kutangaza nia ya nafasi hiyo kubwa kwamba atakuwa amesoma Katiba ya chama, kwahiyo tunaamini kwamba hakuna mtu atakayekiuka utaratibu huo".

Haya yote yanajiri kufuatia mwanamama anayejulikana kwa jina la Dkt Mayrose Majinge, kutangaza nia ya kugombea nafasi ya Urais kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).