Jumatano , 5th Mei , 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu, amesema kuwa serikali imeanza mchakato wa kutafakari mbinu juu ya namna ya kukabiliana na ugonjwa wa Corona, na kusisitiza kuwa wataalamu watakapotoa mapendekezo haitosta kushirikiana na Kenya katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Rais Samia Suluhu Hassan, akihutubia Bunge la Kenya

Kauli hiyo ameitoa hii leo Mei 5, 2021, nchini Kenya wakati alipohutubia mabunge mawili ya nchi hiyo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kuimarisha mahusiano kati ya nchi hizo mbili ambayo ameihitimisha hii leo.

"Tanzania sio kisiwa, kupitia kamati ya wataalamu niliyoiunda tumeanza mchakato wa kutafakari mbinu zaidi za kukabiliana na Corona wakati tunaendelea kusubiri mapendekezo ya wataalam tahadhari zote ikiwemo kusitisha safari kwenye maeneo ya milipuko zinachukuliwa kwa vyovyote itakavyopendekezwa lazima tushirikiane", amesema Rais Samia.

Aidha katika kudumisha mahusiano na nchi jirani, Rais Samia amesema "Rais Uhuru Kenyatta ni mtu wa kutimiza ahadi ili kuondoa mitazamo hasi tumepanga kukutana mara kwa mara maana ndugu wanaotembeleana hujenga ukaribu kuliko wasiotembeleana, umbali hujenga mashaka na ukaribu huondoa mashaka".