Jumanne , 12th Nov , 2019

Msanii na mtayarishaji wa filamu Single Mtambalike, amewakataza watu kusema kuwa wasanii wa  BongoFleva, wamekuja kuchukua nafasi zao kutokana na kuwepo kwa wimbi la baadhi ya wasanii hao kuanza kuigiza filamu.

Msanii na mtayarishaji wa filamu Single Mtambalike.

Kupitia EATV & EA Radio Digital, Single Mtambalike amesema, fani ya kuigiza ina kila mtu na sio ya BongoMovie peke yao.

"Mimi nataka wasiwe wanasema hivyo kwenye masuala yao, huwa nachukia sana, kuhusu kuja kuchukua nafasi zetu kwani sisi ni nani, sisi hapa sio kwetu hii Tanzania ina wenyewe na uigizaji una kila mtu, hakuna mwenye nayo, hata kwenye muziki kulikuwa na kina T.I.D sasa hivi kuna wengine" amesema Single Mtambalike.

Aidha Single Mtambalike ameongeza kuwa, "Kila mtu ana wakati wake kama wakija huku na kufanya vizuri  itakuwa ni wakati wao kufanya hivyo, tukiwa sisi itakuwa hivyohivyo pia, mimi nasema waje tu tena Mungu awajaalie wafanye vizuri, hata sisi heshima yetu itakuwa bado inakumbukwa ila isije kufa kabisa kwa sababu tutasahaulika".

Baadhi ya wasanii ambao sasa hivi wanafanya filamu ni Lulu Diva, Nandy, Quick Rocka, Alice Kella na Gigy Money.