Alhamisi , 7th Mar , 2019

Jaji Sam Rumanyika, amesema Mahakama imeikubali rufani ya viongozi wa CHADEMA, Mwenyekiti Freeman Mbowe pamoja na Muweka Hazina wa Chama, Esther Matiko ambapo amewapatia dhamana.

Mbowe kushoto akiwa pamoja na Esther Matiko

Wakati akitoa uamuzi wa rufaa leo, Jaji Rumanyika amesema kwamba uamuzi uliofanywa na Mahakama ya Kisutu ulikuwa wa mapema mno (Pre - Mature).

Katika chumba cha Jaji Rumanyika, hizi ni kauli ambazo zilitawala kabla ya kutoa maamuzi ya kuwaachia huru viongozi hao baadhi ni hizi.

Kauli ya kwanza: “ Hii ni rufaa mojawapo sijawahi kuiona Katika kazi yangu ya Ujaji. Maofisa wa mahakama kama mahakimu wanapaswa kutumia utashi wao kuamua haki za watu kwa kuzingatia haki", amesema Jaji Rumanyika.

Ya pili: "Ni bora mahakama ikosee kumpa mtu dhamana asiyo sitahili kuliko kumnyang'anya mtu uhuru na haki yake anayostahili".

Ya tatu: "Dhamana ni faraja ya kimahakama, anayeitoa hawezi kuichukua kwa matakwa yake".

“ Hakuna mahala popote warufani wamezuiwa kusafiri Lakini Wakati huo huo wanatakiwa kuripoti Polisi kila Juma. Hii maana yake wamenyimwa Uhuru wa kusafiri na haki ya kufanya kazi".

Ya nne: “Mahakama ya Kisutu ilikabidhi jukumu lake kwa Polisi, sharti la kuripoti polisi kila alhamisi limefutwa badala yake watariporti mahakamani mara moja kwa mwezi si polisi tena ".

Ya tano: “Ni hatari sana kunyima dhamana mtu bila sababu za Msingi".

Ya Sita : "Mbowe na Matiko waachiwe huru mara moja" - Jaji Rumanyika

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu chini ya aliyekuwa Hakimu kwa wakati huo, Wilbard Mashauri, iliwafutiwa Mbowe na Matiko dhamana kwa madai ya kukiuka masharti ya dhamana hiyo ambapo walikata rufaa Mahakama Kuu Desemba 2018, na hatimaye uamuzi wake kutolewa leo.