Alhamisi , 14th Feb , 2019

Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa CHADEMA, Bensoni Kigaila amehoji kati ya Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Simon Sirro nani atakuwa mkweli kuhusiana na uchunguzi wa shambulio la Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu.

Kushoto, IGP Sirro, Katikati ni Benson Kigaila na mwisho ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola

Bw. Kigaila amehoji hayo leo mchana Februari 14, wakati akizungumza na vyombo vya habari kutokana na kauli ya Waziri Kangi kusema kwamba shambulio la Lissu haliwezi kufanyiwa uchunguzi kutokana na kwamba kiongozi huyo kuwa mbali na nchi.

Kigaila amekumbusha kwamba kauli ya Waziri Lugola inakinzana na ile ya IGP Sirro ambaye mara  baada ya tukio la Lissu alisikika akisema kwamba tayari amekwishatuma makachero wake jijini Nairobi kumhoji Lissu.

"Leo Lugola anasema kwamba hawezi kutuma makachero wake nje. Sasa kwahiyo IGP alikuwa anadanganya? na kama alikuwa akidanganya alikuwa anadanganya kwa maslahi ya nani? ni kwanini shambulio la Lissu limekuwa na uwongo mwingi?", amehoji Kigaila.

Mbali na ushahidi wa Lissu, Kigaila amehoji ni kwanini mpaka sasa serikali haijawahoji mfanyakazi wa Naibu Spika, Askari waliokuwa lindoni siku Lissu anapigwa risasi  au kufanya uchunguzi  wa aina ya risasi na kisha kuja kuchukua ushahidi wa mwisho kwa waathirika ambapo ni Lissu na dereva wake.

Kuhusu ziara ya Lissu huko nchi za nje,Kigaila amesema kwamba chama chake kimebariki Mbunge huyo kwa asilimia zote katika ziara zake za nchini Marekani na huko Ulaya kwa kuwa dunia inapaswa kujua jambo Lissu alilotendewa.