Jumatatu , 19th Aug , 2019

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma, imeanza kusikiliza shauri la awali la makosa saba, likiwamo la kubaka mara sita na kumpa mimba mwanafunzi, yanayomkabili Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyantore, Janson Rwekaza.

Akisomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu mkazi Kigoma, Frola Mtarania, Mwendesha mashtaka wa Serikali Clement Masua, amesema mshtakiwa alikuwa na mahusiano na mwanafunzi ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 17 tangu mwezi Mei 2017, akiwa darasa la 5.

Katika makosa hayi Mwalimu Mkuu huyo anatuhumiwa kufanya mapenzi na mwanafunzi huyo mara 6, ikiwemo tarehe 7 na 6 na tarehe 16 mwezi wa nane, 2017, tarehe nyingine ni 10 Julai, 22 Agosti, 2018, pamoja na 3 Februari, 2019 na mwishowe  kumpa mimba mwanafunzi huyo.

Mshtakiwa amekana mashtaka yote saba na yuko nje kwa dhamana huku shauri hilo likiahirishwa hadi Agosti 26, 2019.