Kinachoendelea kesi ya kuua na kumchoma moto mke

Jumanne , 10th Sep , 2019

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, leo Septemba 10 ilikuwa inaendelea kusikiliza kesi ya mauaji inayomkabili mfanyabiashara Khamis Saidy, anayekabiliwa na mashtaka ya kumuua na kisha  kumchoma moto Mke wake.

Mfanyabaishara Khamis Saidy anayekabiliwa na mashtaka ya mauaji akiwa Mahakamani.

Akizungumza Mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Salum Ally, Wakili wa Serikali Wankyo Simon amesema kuwa, upelelezi wa kesi hiyo upo katika hatua za mwisho ili kuipatia mahakama hiyo nyaraka na hatimae kesi hiyo kupelekwa Mahakama Kuu.

Kufuatia maelezo hayo, mshtakiwa aliomba kupatiwa hati ya mashtaka yanayomkabili ambapo wakili Wankyo, aliahidi kumpatia na kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 24, itakapofikishwa mahakamani hapo tena kwa ajili ya kutajwa.

Mfanyabiashara huyo anakabiliwa na mashtaka ya kuua kwa kukusudia, ambapo inaelezwa alitekeleza kosa hilo Mei 15, 2019, mara baada ya kumuua kisha kumchoma na moto wa magunia mawili ya mkaa mke wake Naomi Marijani, kisha kuyachukua mabaki ya mwili huo na kwenda kuyafukia shambani kwake Mkuranga.