Jumatatu , 16th Mei , 2016

Ugonjwa wa Kipindupindu umeendelea kupoteza uhai wa watanzania kwa muda wa miezi 7 sasa bila kudhibitiwa ambapo kwa mwezi huu idadi ya waathirika wapya wa ugonjwa huo wamefikia watu 212 kwa nchi nzima, tayari watu 338 wamepoteza maisha tangu mlipuko.

Waathirika wapya wa ugonjwa huo wamefikia watu 212 kwa nchi nzima na kuwa tayari watu 338 wamepoteza maisha tangu kugundulika kwa ugonjwa huo.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto inaeleza kuwa kwa mwezi Mei watu 212 wamebainika kuwa na ugonjwa huo kutoka wagonjwa 138 walioripotiwa kwa mwezi Aprili mwaka huu ambapo watu watano 5 wamepoteza maisha.

Mkoa wa Morogoro unaongoza kwa kuathiriwa ikiwa na wagonjwa 78, ikifuatiwa na mkoa wa Lindi yenye wagonjwa 51, mikoa mingone ni pamoja na mkoa wa Dar es Salaam ambako ugonjwa huo umepungua kwa mwezi huu kwa kuwa na wagonjwa 16, ukifuatiwa na mkoa wa Mara, Pwani na Kilimanjaro.

Halmashauri zilizoongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi katika wiki hiyo iliyopita ni Kilwa (51), Kilosa (47), Babati Vijijini (33), Mvomero (23), Kinondoni (10), Mbulu (9), Kibaha Mjini (8), Morogoro Mjini (8), Tarime Mjini (8), Same (6), Temeke (6) na Bukoba Mjini (3). Halmashauri 4 ziliripoti vifo vilivyotokana na ugonjwa huu; Kilwa (2), Mvomero (1), Tarime Mjini (1) na Bukoba Mjini (1).

Aidha viongozi wa Vijiji, Mitaa na Kata ambako bado wanasumbuliwa na ugonjwa huo na jamii kwa ujumla wametakiwa kushiriki kikamilifu kuweka mazingira yao katika hali ya usafi ili kuepusha vifo visivyo vya lazima vitokanavyo na ugonjwa huo.

Katika mahojiano na wananchi juu ya ugonjwa huo mmoja wa wananchi Bw. Abdalah Ally amesema serikali ihakikishe kuwa miundombinu ya majitaka na vyoo kote nchini inazingatia sifa za usafi ili kuwalinda mamia ya wananchi wanaopoteza maisha kwa ugonjwa huo.