Kitila Mkumbo aanika ukweli

Thursday , 12th Oct , 2017

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na umwagiliaji Profesa Kitila Mkumbo, ameweka wazi sababu ya yeye kukubali kuteuliwa kushika wadhifa huo, licha ya misimamo ambayo alikuwa nayo awali, dhidi ya wasomi wanaoteuliwa kushika wadhifa mkubwa serikalini.

Akizungumza kwenye kipindi cha East Africa Breakfast kinachorushwa na East Africa Radio, Prof. Mkumbo amesema kilichofanyika kwake ni kupandishwa cheo kutoka nafasi aliyokuwa nayo awali, na asingeweza kukataa kwani ni heshima kubwa aliyopewa na Rais.

“Wakati nimeteuliwa na Rais, mimi nilikuwa mtumishi wa umma, nilipandishwa cheo kutoka chuuo kikuu mpaka ukatibu mkuu, nani huyo akipandishwa cheo atakataa!!? Mimi nilikuwa mtumishi wa umma, hiyo ni heshima kubwa niliyopewa”, amesema Kitila Mkumbo

Prof. Mkumbo ameendelea kwa kusema kwamba baada ya kuteuliwa huko hakuchelewa kuachia wadhifa ambao alikuwa nao kwenye chama cha ACT- Wazalendo, kwa kuwa aliona dhahiri asingeweza kuendeleza harakati alizokuwa anafanya kwenye chama.

“Katika nafasi ya Katibu mkuu, mimi sio tu mtumishi wa umma, mimi ni serikali nawajibika kwa serikali kuisimamia, kutekeleza mipango ya serikali, tofauti kabisa na uhadhiri, kwenye chama nilikuwa nafanya harakati, nikaona hili sasa haliwezekani, ikabidi niwaombe wenzangu kwamba hapa nilipofika majukumu haya siwezi kuchanganya na uanachama wangu, ikabidi niweke uanachama pembeni”, amesema Kitila Mkumbo.

Hivi karibuni Kitila Mkumbo amejiondoa unachama wa ACT- Wazalendo, akisema kwamba hatoweza kutumikia serikali akiwa mwananchama wa chama hicho, kwani kuna mgongano wa maslahi.