Kodi ya majengo kukusanywa kupitia LUKU

Alhamisi , 10th Jun , 2021

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, amependekeza kuwa ukusanyaji wa kodi za majengo ufanyike kwa kutumia mfumo wa ununuzi na utumiaji wa umeme kupitia mashine za LUKU.

LUKU

Mapendekezo hayo ameyatoa leo Juni 10, 2021, wakati akiwasilisha makadirio na matumizi ya bajeti ya kuu serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022 aliyoiwasilisha Bungeni hii leo.

"Kila mita ya umeme ina uhusiano na mmiliki wa jengo na kwa kuwa sheria ya kodi ya majengo inataka kodi hiyo ikusanywe kwa mmiliki au mtumiaji wa jengo, hivyo, napendekeza kodi ya majengo ya kiwango cha shilingi 1,000 kwa mwezi kwenye nyumba za kawaida zenye mita moja na itakatwa kwenye ununuzi wa umeme,"ameeleza Dkt. Nchemba.

"Aidha, amependekeza kiwango cha shilingi 5,000 kwa mwezi kwa kila ghorofa au apartment zenye mita moja na itakatwa kwenye ununuzi wa umeme (LUKU), serikali itaweka utaratibu kwenye nyumba za kawaida na za ghorofa zinazochangia mita moja na zinazotumia mita zaidi ya moja," ameongeza Waziri Dkt. Nchemba.