Kubenea amtolea uvivu Sakaya

Friday , 14th Jul , 2017

Kaimu Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani CHADEMA , Saed Kubenea amemtolea uvivu mbunge wa jimbo la Kaliua Magdalena Sakaya kwa kudai CHADEMA haijaingilia ugomvi wa chama chao bali wanataka kumaliza mgogoro uliopo kwa kuwaondoa mamluki.

Akizungumza na Wanahabari Mh. Kubenea amesema kwamba CHADEMA imeamua kujitosa katika mgogoro wao baada ya kuombwa na wabunge wa chama hiko wakiongozwa na viongozi waandamizi akiwepo Maalim Seif Sharif Hamad.

"Sakaya ananituhumu  na kusema CHADEMA tunawaingilia CUF, nataka niseme kwamba hatujaingilia ugomvi wao, pili Sakaya siyo mwanachama wa CUF kwani alikwisha vuliwa uanachama na akafukuzwa, pia hana uongozi wowote ndani ya chama hicho kwani hata barua yake ya rufaa mpaka leo haijakubalika, na Naibu Katibu Mkuu mimi ninayemtambua ni Bashange na siyo yeye" Kubenea.

Aidha Kubenea ameongeza kuwa

"Matukio yote ambayo CUF wamekuwa wakitendeana  kama Lipumba na genge lake kuvamia mkutano CHADEMA hatukuwepo, sasa kwa vile wameomba msaada kwetu sisi tumeanzisha oparesheni ondoa msaliti Buguruni ambayo tutaifanya kwa ukamilifu. Tumeagizwa na kamati kuu kuikomboa CUF", aliongeza Kubenea.

Pamoja na hayo Kubenea amesema lengo la CHADEMA kumsaidia Maalim Seif vita yake na Prof. Lipumba ni kuinusuru chama chao kilichopo ndani ya mwamvuli wa UKAWA kisije kikaingia kwenye migogoro inayosababishwa na CCM ili kuua upinzani ndani ya Tanzania.