Jumatatu , 15th Oct , 2018

Uchaguzi wa Naibu Meya wa jiji la Dar es salaam umelazimika kuahirishwa kutokana na wajumbe wa mkutano huo kutoafikiana kwa baadhi ya vipengele, ikiwemo kutokukubaliwa kwa hati ya mgombea wa nafasi hiyo aliyetokea (UKAWA) kupitia Chama Cha Wananchi CUF.

Katika mkutano huo ilishuhudiwa baadhi ya wajumbe akiwemo Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea wakiingia kwenye malumbano ya maneno na Mkurugenzi wa Jiji, Sipora Riama juu ya hati ya mgombea huyo.

"Tunaomba hoja iliyotolewa na mjumbe Ndugulile aipokee Mkurugenzi na aseme ameikubali ili twende mbele, mheshimiwa ndugulile  tumuulize Mkurugenzi amekubali kuja na utaratibu mpya kwenye kikao kijacho", amesema Kubenea.

"Kwanini unaingilia majukumu yangu, huyu naye ni (Meya wa jiji) ana maslahi hawezi kutoa miongozo, mimi nina wanasheria hapa, maafisa utumishi ili kusimamia uchaguzi na miongozo mimi ndo natoa", amesema Sipora wakati akizungumza kwa sauti kwenye kikao hicho.

"Nimshukuru Mheshimiwa Ndugulile, kwa kuwa tumekubaliana kuhairisha kikao, naomba UKAWA kupitia chama cha wananchi CUF kipate haki yake ya kupata mgombea wake, tunaomba kikao kinachokuja ajenda moja wapo iwe ni uchaguzi", amesema Mdee kwa kumalizia.

Awali Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Wazee na Watoto, Dkt Faustine Ndugulile alitoa ushauri wa kuhairishwa kwa ajenda ya uchaguzi kwenye kikao hicho, hoja ambayo ilikuja kukubaliwa mwishoni mwa kikao.

"Kikao chetu kimedumu kwa zaidi ya saa 4 kitu ambacho nakiona hapa, kitu ninachokiona hapa mjaala huu haitafika mwisho, naomba tuhairishe ajenda ya uchaguzi mpaka siku nyingine"