Kutekwa kwa MO Dewji, Makonda afunguka hili

Alhamisi , 11th Oct , 2018

Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda, ametaka kufungwa kwa kamera katika maeneo yote jijini Dar es salam, ili kupata msaada mkubwa yanapotokea matukio ya kiuhalifu.

Akizungumza na waandishi wa habari walipofika eneo la tukio alipochukuliwa mfanya biashara mkubwa Afrika Mashariki, Mohamedi Dewji, Paul Makonda amesema iwapo Dar es salaam itafungwa kamera, itakuwa msaada mkubwa kwa vyombo vya usalama kufuatilia matukio ya kiuhalifu kama la kutekwa kwa Mo Dewji.

“Tuna mpango mkubwa zaidi nafikiri umefika wakati sasa wa mkoa wa Dar es salaam wote kufungwa camera, leo hii tungekuwa na camera, tungeongezea hata weledi wa jeshi letu la Polisi kufuatilia gari iko wapi, ifike hatua Dar es salaam iwe na camera tukamate wahalifu kwa haraka zaidi, kuliko kutumia nguvu kubwa kumfuatilia mtu ambaye hujui amepita wapi”, amesema Paul Makonda.

Paul Makonda ameendelea kwa kusema kwamba kamera hizo zitafungwa kwenye mahoteli yote makubwa, shopping mall, na barabarani, ili kusaidia suala la ulinzi na usalama, na kuwataka wananchi kutoa taarifa zozote watakazopata kuhsu tukio hilo.

Mohamed Dewji ametekwa na watu waliofahamika kuwa ni rai wa kigeni (wazungu) mapema leo asubuhi, alipokuwa ameenda kufanya mazoezi katika hoteli ya Colloseum jijini Dar es salaam.