Kuungua kwa shule za Kiislamu, Waziri atoa neno

Ijumaa , 31st Jul , 2020

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa kutokana na kufululiza kwa matukio ya kuungua kwa shule za kiislamu jijini Dar es saalam, tayari Mkuu wa Mkoa huo Abubakar Kunenge ameunda kamati za uchunguzi ili kubaini chanzo cha matukio hayo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Waziri Mkuu amesema hayo wakati akizungumza katika  Baraza la Eid El Adh’haa  lililofanyika Kitaifa kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, na kuongozwa na Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir Bin Ally ,leo Julai 31, 2020, ambapo amewaasa waumini hao pia kusherekea sikukuu hiyo kwa amani.

Waziri Mkuu amesema kuwa inashangaza kwanini matukio hayo yajitokeze kwa shule za kiislam pekee, hivyo viongozi wa Mkoa wahakikishe wanapata chanzo cha matukio hayo, ili kuondoa sintofahamu hiyo.

“Hizi shule wanasoma wanafunzi wa dini zote na hakuna ubaguzi wowote nchini, ila haya matukio yamefatana Mkoa wa Dar es salaam, tayari Mkuu wa Mkoa ameshaunda kamati ya uchunguzi na italeta majibu haraka iwezekanavyo”, amesema Waziri Majaliwa.

Kwa upande wake Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir, amewataka waumini wa kiislamu kutumia siku hiyo kutoa sadaka kwa watu wasiojiweza ili wote washerehekee kwa pamoja.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ambao ndiyo mwenyeji wa swala hiyo kitaifa, Abubakar Kunenge, amewataka wakazi wa mkoa huo kusherehekea sikukuu hiyo kwa kiasi na wasiwe chanzo cha migogoro.