Lema aeleza polisi walivyotaka kumdaka hotelini

Jumapili , 29th Mar , 2020

Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, amesema kuwa hadi sasa hajajua ni kwanini alizingirwa na polisi alipokuwa hotelini, licha ya kuwasiliana na Makamanda wa Polisi wa Mikoa husika, ambao na wao hawakuweza kumpa sababu ya msingi.

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema

Akizungumza na EATV&EA Radio Digital, Lema amesema kuwa hakuona sababu yoyote ya polisi kumzingira sehemu ya watu ya biashara, kwani ilisababisha hofu kwa wateja na wageni katika eneo hilo, hivyo ni vyema wangempigia hata simu angeweza kujisalimisha mwenyewe kituo cha polisi.

"Ni kweli nilizingirwa na polisi hotelini lakini bahati nzuri hawakufanikiwa kunikamata, lakini nilifuatilia kwa Kaimu RCO Kinondoni akaniambia tutaongea baadaye na hakuniambia chochote, na mimi nilijua labda kulikuwa na jambo ambalo walikurupuka" amesema Lema.

Machi 17, 2020, kupitia kwa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa CHADEMA Tumaini Makene, alizungumza na EATV Digital na kutoa taarifa za kuwa Mbunge Lema amezingirwa na Askari Polisi katika hoteli ya Regency Park iliyoko Mikocheni.