Alhamisi , 14th Nov , 2019

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, ameeleza sababu iliyofanya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kukamatwa na Polisi wilayani humo kwa kuwa alikuwa anafanya siasa za kihalifu na zenye mlengo wa kuleta taharuki kwa wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.

Akizungumza na EATV&EA Radio Digital, leo Novemba 14, 2019, Sabaya amesema kuwa Lema alifika wilayani hapo na kufanya kikao cha siri na viongozi wenzake wa CHADEMA chenye lengo la kuwashawishi wananchi kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kinyume cha taratibu ilihali yeye si Mbunge wa eneo hilo.

"Tunataka kumuonesha, kiufupi hapa Hai sio salama kabisa kwa watu wahalifu kufanya siasa, kwakuwa hali hiyo ilikuwa inataka kuleta taharuki kwa wananchi, tutaangalia sheria inasemaje na hatua zingine zitafuata,wananchi wa Hai hawamjui Lema ni nani, yeye amekutana na viongozi wenzake kufanya hivyo na ndio maana hata Polisi walipofika hapo hakujisalimisha aliruka ukuta na kukimbia, hadi alipokuja kukamatwa baadae tena, yeye aende kwa wananchi wake wa Arusha  akaongee nao juu ya kuwapunguzia ukali wa maisha" amesema DC Sabaya.

Kwa mujibu wa DC Sabaya, Lema pamoja na Mwenyekiti wilayani humo Helga Mchomvu,  wamekamatwa leo Novemba 14, kwa makosa ya kufanya mkutano usio halali.