Jumatano , 18th Apr , 2018

Serikali ya awamu ya tano kupitia Wizara ya Nchi Ofisi ya Utumishi na Utawala Bora imesema haioni haja ya kubadilisha sheria iliyopo ya uzazi kwa sasa, kwasababu inampa fursa mwanamke kupumzika kutozaa mara kwa mara na kufuata uzazi wa mpango kama nchi inavyoelekeza nasio vinginevyo.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Wizara hiyo, George Mkuchika leo Aprili 18 Bungeni jijini Dodoma kwenye kikao cha 12 mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalum Sonia Juma Magogo aliyetaka kufahamu mpango wa serikali wa kutaka kuwasaidia wakina mama ambao wanajifungua kabla ya kipindi cha kuruhusiwa kupata miezi mitatu ya mapumziko ili waweze kuwanyonyesha vichanga hivyo na kuendelea majugumu yao ya kiofisi ?.

"Kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2009. Mtumishi wa umma anapojifungua hupewa likizo ya malipo ya siku 84 na iwapo atajifungua zaidi ya mtoto mmoja (mapacha) ataongezewa siku 14 na kuwa jumla ya 98. Endapo mtumishi atajifungua mtoto tena kabla ya kutimiza miaka mitatu atapewa likizo maalum ya wiki sita ili kuhudumia mtoto wake kwa mujibu wa kanuni na baada ya hapo serikali inaweza kumuongezea siku za kupumzika kulingana na ushauri wa daktari", amesema Mkuchika.

Pamoja na hayo, Waziri Mkuchika ameendelea kwa kusema "likizo ya uzazi hutolewa mara moja katika kipindi cha miaka mitatu kwa kuzingatia sera ya afya ya mama na mtoto inayosisitiza kulinda na kujenga afya ya mama na mtoto na kuhimiza uzazi wa mpango. Sheria hizi ni za nchi nzima hivyo zinapaswa ziheshimiwe na kufuatwa kwa wale waliokoa serikali na mashirika ya umma.

Kwa upande mwingine, Waziri George Mkuchika, ametoa rai kwa watumishi wa umma au sekta binafsi, kuwa endapo yeyote atakayenyimwa haki ya likizo ya uzazi basi aitaarifu Wizara husika ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mwajiri wake.