Jumanne , 19th Mar , 2019

Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi CUF, Prof Ibrahim Lipumba amewaomba wanachama wa chake upande wa Zanzibar kuendelea kusalia kwenye chama hicho licha ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif kutangaza kuhamia ACT - Wazalendo.

Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi CUF, Prof Ibrahim Lipumba

Prof Lipumba ametoa kauli hiyo Jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya hali ya mgogoro wa chama hicho ambao Mahakama ilimpatia haki ya kuendelea kuwa Mwenyekiti wake.

Lipumba amesema, "ndugu wa Zanzibar ninachowaambia CUF mliijenga kwa muda mrefu, ndiyo maana CUF, ilikuwa na wimbo wa taifa wa chama, sasa Maalim Seif ACT ataimba nini".

"Niwaambie tu ndugu zangu wa Zanzibar kuchoma bendera ya chama chochote ni kosa la jinai nawaomba waache.", ameongeza Lipumba.

Pia Lipumba amesema, "ni kosa la jinai ofisi ya CUF kuitambulisha kuwa ofisi ya ACT - Wazalendo, akili za kuambiwa changanya na zako Maalim Seif anaweza kukwambia ubadilishe halafu mwisho akakuacha peke yako" amesema Lipumba

Mgogoro wa CUF umedumu kwa zaidi ya miaka 3, lakini jana Machi 2019, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es salaam ikatoa uamuzi uliompa ushindi Profesa Ibrahim Lipumba.