Ijumaa , 19th Apr , 2019

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Antiphas Lissu, amesema kilichofanya Bunge la Tanzania kumpatia mshahara wake ni jinsi ambavyo watanzania waliamua kuwa majasiri na kumchangia mshahara wake.

Mbunge Tundu Lissu

Kupitia waraka wake maalum ambao amekuwa akiutoa mara kwa mara kuhusiana na mwenendo wa afya yake Tundu Lissu amesema kwamba bunge limelipa mshahara wake kuanzia mwezi Januari hadi Machi.

Kwa maoni yangu, kilichowafanya wakubali yaishe ni ujasiri wa watu wengine mlioamua kunichangia, siyo tu gharama za matibabu yangu, bali hata huo mshahara uliozuiliwa kinyume na sheria na kanuni za Bunge,” amesema

Ameongeza kwamba, “sikukubali kufa kimyakimya na nyinyi ndugu zangu hamkukubali. Walipoona sokomoko la mshahara wangu limekuwa kubwa na sasa limebebwa na wananchi, wakakubali yaishe. Nawapongezeni sana kwa ushindi huu".

Lissu kwa sasa anapatiwa matibabu nchini Ubelgiji kufuatia kushambuliwa kwa risasi alipokuwa kwenye muendelezo wa vikao vya Bunge jijini Dodoma Septemba 2017.