Ijumaa , 17th Aug , 2018

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, ametoa wiki moja kwa polisi wilayani Bunda, mkoani Mara, kuwakamata wanafunzi watoro na wazazi wao, pamoja na wanaowarubuni wanafunzi wa kike na kuwasababishia kukatisha masomo.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, akizungumza na wananchi wa jimbo la Mwibara ambalo ndio analoliongoza lililopo wilayani Bunda.

Lugola, amesema kiwango cha wanafunzi kuacha masomo kinazidi kuongezeka hivyo serikali haiwezi kukaa kimya, lazima ifanye kitu kuhakikisha wanafunzi hao wanasoma ili waje kuwa viongozi wa nchi.

Lugola, ametoa kauli hiyo  akiwa wilayani humo katika  ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo ndani ya jimbo lake la Mwibara, ambapo amesema kuwa anasikitishwa na idadi kubwa ya wanafunzi walioacha shule wilayani humo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kurubuniwa na wanaume.

 “Nawapa wiki moja Mkuu wa Polisi hapa Bunda mtumie elimu zenu za upelelezi mlizofundishwa, wahojini ndugu, wachunguzeni,  wakamateni, jamaa, majirani mtawapata wote wanaowarubuni wanafunzi, halafu mshughulike nao,” ameagiza Lugola.

Kwa mujibu wa Takwimu zilizotolewa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Watoto wa wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto,  Margret Mussa  mwaka 2017 wakati wa maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya mtoto wa kike ambayo huadhimishwa Oktoba 11, kila mwaka zilionesha kuwa kasi ya ufungaji wa ndoa za utotoni kwa mkoa wa Shinyanga ni asilimia 59%, Tabora (58%), Mara (55%), Dar es Salaam (17%) na Iringa (8% ).

Pia, takwimu hizo zilionyesha kuwa wasichana 36 kati ya 100 huolewa kabla ya wakati huku 27 kati ya 100 wakipata ujauzito wakiwa chini ya umri wa miaka 18 kila mwaka