Madereva walio-bet uhai wa watu kufutiwa sifa

Ijumaa , 26th Jun , 2020

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Fortunatus Muslimu, amesema kuwa madereva wawili wa mabasi ambao video yao ilisambaa mitandaoni wakishindana barabarani, atawachukulia hatua za kuwaondolea sifa za kuendesha magari hayo, kuwafungia kwa miezi 6 pamoja na kuwapeleka mahakamani.

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Muslimu.

Kamanda Muslimu ametoa kauli hiyo leo Juni 26, 2020, wakati akizungumza kwenye kipindi cha SupaBreakfast ya East Africa Radio na kuongeza kuwa Jeshi hilo limebaini kuwa madereva hao walikuwa wame-bet ili kuona ni nani atakuwa wa kwanza kufika kwenye kituo fulani.

"Nimechukua hatua kali sana, tumewakamata wote na wako ndani na tumeandaa utaratibu wa kisheria ikiwemo kuwafikisha Mahakamani, Sheria inanipa uwezo wa kuwaondolea sifa wa kuendesha haya magari ya mizigo na biashara na kwa miezi 6 hawa hawatokuwa barabarani wakiendesha Mabasi wala Malori labda hivi vigari vidogo" amesema Kamanda Muslimu.

Jana ilisambaa video mitandaoni ikionesha Madereva wa Mabasi ya Happy Nation na Rugwe, wakikimbizana barabarani bila kujali usalama wao wala abiria waliokuwa nao.