Jumapili , 18th Aug , 2019

LABDA naye afe katika tukio la ajali iliyotokea, lakini kama atabahatika kuwa hai baada ya ajali ya gari la serikali lililosababisha kifo au vifo vya watumishi wengine wa serikali, dereva wa gari hilo ndiye atakayebeba msalaba wa uwajibikaji ikiwemo kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Moja ya ajali iliyohusisha gari za serikali

Ajali za magari ya serikali imekua ni jambo lisiloshtua kusikika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Imekuwa kawaida kusikia watumishi wa serikali wawili, watatu, wanne mpaka watano wamekufa kwa ajali ya barabarani. Huku Jeshi la Polisi likisema karibu ajali zote zinazotokea zikihusisha magari ya serikali zinatokana na mwendokasi pamoja na uchovu wa madereva.

Hakuna sababu zingine za ajali ya magari ya serikali. Ni kujiamini kupitiliza kwa madereva kwamba hawawezi kuchukuliwa hatua yoyote ya kisheria pale watakapovunja sheria ikiwemo kuzidisha mwendo unaokubalika kisheria. Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP)", Deus Sokoni ambaye ni Mkuu Kitengo cha Sheria cha Kikosi cha Usalama Barabarani anamwambia mwandishi.

"Mwendo sahihi wa gari kisheria unatajwa kifungu cha 51 cha Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, ya kwamba ni kilometa 50 kwa saa katika maeneo ya makazi ya watu, lakini maeneo yenye vibao vinavyoelekeza mwendo madereva wanalazimika kufuata maelekezo lakini katika maeneo yasiyo ya makazi na yasiyo na vibao dereva wa gari chini ya uzito wa tani 3.5 anaruhusiwa kwenda mwendo wowote autakao lakini magari yaliyo juu ya uzito huo yakitakiwa kutozidisha kilometa 80 kwa saa".

Baadhi ya ajali za magari ya serikali zilizotokea na kuzua mjadala mkali kutokana na mazingira ya ajali hizo ni ile iliyomhusisha Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamis Kingwangalla, iliyotokea Agosti 4, 2018 eneo la Magugu, mkoa wa Manyara na kusababisha kifo cha ofisa habari wa wizara hiyo Hamza Temba huku waziri mwenyewe akijeruhiwa vibaya, kiasi cha ndege ya kukodi kuitwa kwa dharura ili kumuwahisha kituo cha afya cha Seliani na baadaye kumpeleka hospitali ya Taifa Muhimbili.

Siku moja baada ya ajali hiyo, waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola alijitokeza mbele ya wanahabari akisema, “Sheria imewekwa ili kumlinda kila raia na ndiyo maana leo hii mtu akinywa sumu na akanusurika kufa anashtakiwa, hivyo basi kama wewe kiongozi upo na dereva wako anasababisha ajali kizembe atachukuliwa hatua kali kama ilivyo kwa watu wengine bila kumwonea huruma.”

Mpiga picha wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Michael Mlingwa ambaye alikua miongoni mwa watu wanne kati ya watano walionusurika katika ajali alibainisha kuwa ajali hiyo ilitokea wakati wakiwa katika maeneo yenye wanyama, hivyo Twiga alikatiza ghafla barabarani na wakati dereva akijaribu kumkwepa ndipo magurudumu ya gari yalipasuka na gari kupinduka zaidi ya mara tatu.

Oktoba 21, 2018 ajali ya gari la serikali Na. STK 8925 lililogangana na lori ilisababisha vifo vya watumishi watano wa serikali, wakiwemo wataalamu wanne wa wizara ya kilimo na dereva. Hapa hakuna aliyenusurika. Mkuu wa Polisi Mkoa wa Singida Sweetbert Njewike alieleza kuwa chanzo cha ajali hiyo kuwa ni dereva kutokua makini ikiwemo mwendokasi, lakini siku mbili baadaye aliyekuwa waziri wa Kilimo Dk. Charles Tizeba alijitokeza na kuipinga taarifa ya polisi akisema si ya kweli na kutaka uchunguzi zaidi ufanyike.

...Polisi waende wakafanye utafiti tena kwani kumekua na lawama kwa dereva wa serikali ambazo hazistahili maana taarifa zinasema dereva wa lori ndiye aliyeingia barabrani pasipo kufuata utaratibu, jambo lililosababisha ajali hiyo”, alisema Dk. Tizeba wakati wa shughuli ya kuaga miili ya watumishi wa Wizara ya Kilimo.

Takwimu za polisi zinaonesha zaidi ya watumishi wa serikali 34 wamefariki katika matukio mbalimbali ya ajali za magari ya serikali yaliyotokea mwaka mmoja na nusu uliopita, ikiwa ni wastani wa watumishi wawili wa serikali kufariki kila mwezi kutokana na ajali za barabarani.

Ipo orodha ndefu ya ajali za magari ya serikali ikiwemo ya Mei 21, 2018 Chalinze mkoani Pwani iliyosababisha vifo vya watumishi watatu wa kituo cha uwekezaji nchini (TIC), kupoteza maisha baada ya gari Na. STK. 5923, Toyota Land Cruiser mali ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji likiwa mwendo mkali kugongana na gari aina ya Scania.

Julai 14, 2018 ilitokea ajali ya gari la Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, ambalo liliacha njia na kupinduka mkoani Singida na kusababisha vifo viwili na majeruhi watano, polisi wakisema chanzo kilikuwa mwendokasi uliosababisha kupasuka kwa gurudumu mbele na gari hilo kupinduka baada ya kuacha njia.

Ajali ya Julai 30, 2018 Katoro mkoani Geita baada ya gari la serikali kupinduka likimkwepa mtembea kwa miguu, ilisababisha kifo cha Shadrack Sagati, Ofisa Habari Wizara ya Viwanda huku Naibu Katibu Mkuu wa Wizara na maofisa wengine watano wakijeruhiwa.

Novemba 3, 2018 ajali ya magari mawili ya serikali ilisababisha vifo vya watu saba, ikiwemo watumishi wa ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Kongwa, mkoani Dodoma huku Kamanda wa Polisi mkoani humo, Gilesi Muroto akieleza kuwa chanzo cha ajali kilikua mwendokasi.

Februari 23, 2019 ajali ya gari la serikali iliua maofisa ardhi tisa, Ifakara mkoani Morogoro Jeshi la Polisi likieleza kuwa gari ya serikali ilikua kwenye mwendo mkali kabla ya kutumbukia mtoni baada ya kumshinda dereva. Julai 27, 2019 gari la polisi PT 3822 lilipasuka gurudumu la nyuma na kupinduka maeneo ya Mkuranga mkoani Pwani huku askari watatu wakipoteza maisha.

Juni 25, 2019 pia gari Na. STL 3807 Toyota Hilux la Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) mkoa wa Songwe ilisababisha vifo vya watu wawili na majeruhi watatu katika kata ya Izazi Tarafa ya Isimani, ambayo ni Barabara Kuu ya Iringa – Dodoma mkoani Iringa.

Julai 25, mwaka huu askari watatu wa Jeshi la Polisi nchini nao walifariki dunia huku wengine wawili wakijeruhiwa katika ajali ya serikali iliyotokea kijiji cha Kilimahewa, Mkuranga mkoani Pwani baada ya gari lao Na. PT 3822 aina ya Toyota Land Cruiser kupasuka grudumu la upande wa nyuma na kupinduka.

Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya Ulrich Matei ambaye amewahi kuitisha mkutano na madereva wote wa serikali mkoani humo, ambapo aliwakusanya wakaguzi wa magari kutoka jeshi la polisi pamoja na wakufunzi kutoka chuo cha ufundi (VETA), ili kuzungumza na madereva lakini madereva hao walitoa malalamiko kuwa wamekua wakisafiri umbali mrefu bila kupumzika, kuamrishwa kwenda mwendokasi na magari kutokaguliwa na kutengenezwa (service).

Niliwaambia madereva wa magari ya serikali kuwa hawatakiwi kwenda mwendokasi kwa kisingizio kuwa wameamrishwa. Wao ndiyo wanaoendesha na ni wataalamu wanaotakiwa kuchukua jukumu la kuhakikisha wanafika salama pamoja na viongozi wanaowaendesha”, alisema Kamanda Matei huku pia akidokeza kuwa mwaka 2017 mkoani Mbeya zilitokea ajali 10 za magari ya serikali na mwaka 2018 zikitokea ajali 14.

Nilipomuuliza ASP Deus Sokoni, Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa Kikosi cha Usalama Barabarani kuhusu hatua ambazo huchukuliwa kwa madereva au viongozi wanaoamrisha madereva waende mwendokasi na kusababisha ajali za magari ya serikali, alisema, “tunawafungia leseni madereva wote wanaosababisha ajali hizo, kisha tunawafikisha mahakamani.”

ASP Sokoni amesema ingawa wanafahamu kuwa wapo madereva wa serikali ambao huamrishwa kuendesha gari wakiwa wamechoka, na pia kuamrishwa kwenda mwendokasi lakini kukubali kwao kufanya hivyo huku wakijua si sahihi ni uzembe na ujinga hivyo lazima jeshi la polisi liwachukulie hatua za kisheria.

ASP Sokoni ametaja baadhi ya madereva waliofungia leseni zao baada ya kusababisha ajali za magari ya serikali na wao kubaki hai kuwa ni dereva aliyesababisha ajali ya waziri Dk. Kingwangalla, dereva aliyehusika kwenye ajali iliyoua watumishi watatu wa TIC, madereva wa ofisi ya CAG na PSSSF waliogonga mkoani Dodoma, dereva aliyesababisha kifo Sagati, ofisa habari wizara ya viwanda na dereva wa gari lililoua watumishi wa TARURA.

Sheria ya usalama barabarani inaturuhusu kufungia leseni ya dereva. Sisi hatusubiri uamuzi wa mahakama, wala hatujali mahakama itaamuaje kuhusu dereva huyo. Baada ya dereva kumaliza miezi sita ya kufungiwa leseni yake na kutotakiwa kuendesha gari, anafanya upya mtihani wa udereva na anayefeli tunamnyima leseni. Tukishawafungia madereva wa serikali tunaandika barua kwenda kwa waajiri wao kuwajulisha kuwa dereva wao hatakiwi tena kuendesha gari kwasababu hana leseni hivyo wanatafuta dereva mwingine,” anasisitiza ASP Sokoni.

Augustus Fungo, mdau wa usalama barabarani akitoa mtazamo wake kuhusu ajali za magari ya serikali anasema “ajali haijali kama upo kwenye gari la serikali wala la jeshi. Ikishatokea unakufa tu, askari wanatakiwa kusimamisha na kukamata magari ya serikali kama wanavyofanya kwa raia wengine.”

Fungo anasimulia kisa cha gari moja ya serikali iliyosimamishwa mara tatu na ikakataa kusimama, mpaka yaliposimamishwa magari mengine njiani na yenyewe kukosa pa kupita, akitaja kama mfano hai na halisi wa viburi vya madereva wa magari ya serikali.

Askari wamekua wakilalamika kuwa baadhi ya magari ya serikali hayakubali kusimama hata yakisimamishwa na askari na kukamatwa viongozi wanawatetea madereva. Kiongozi anayeendeshwa ana wajibu pia wa kuhakikisha ajali haitokei kwasababu inaweza kugharimu maisha yake na serikali na wananchi kukosa huduma na utaalamu wake,” anasema Fungo.

Ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), ya mwaka 2018 inaitaja Tanzania kama miongoni mwa nchi zinazotumia kiasi kikubwa cha pato lake la Taifa kukabiliana na madhara yatokanayo na ajali za barabarani ambapo zaidi ya asilimia 3 ya pato la Taifa sawa na shilingi trilioni 4 hutumika kwa mwaka.

Ripoti hiyo inasema asilimia 30 za ajali za barabarani katika nchi zilizoendelea hutokanana mwendokasi huku nusu ya ajali katika nchi za dunia ya tatu, Tanzania ikiwemo husababishwa na mwendokasi. Tafiti za WHO zinaeleza zaidi kuwa kadri dereva anavyoongeza mwendo ndivyo uwezekano wa ajali kutokea huongezeka.

Gari linalokimbia kilometa 50 kwa saa litahitaji kusogea mita 13 zaidi mbele ili liweze kusimama na gari linalokimbia kilometa 40 kwa saa litasogea kwa mita 8.5 mbele ndipo liweze kusimama. Kila inapoongezeka kilometa moja kwa saa na uwezekano wa kutokea kwa ajali uonaongezeka kwa asilimia tatu,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.