Alhamisi , 21st Nov , 2019

Madiwani wa Halmashauri ya Chalinze, wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, wameazimia kuchanga kiasi cha shil. Mil. 10, ikiwa ni sehemu ya kumfariji mtoto Anna Zambi, aliyeondokewa na wazazi wake wawili na wadogo zake watatu katika ajali ya gari iliyotokea mkoani Tanga.

Anna Zambi alyepoteza wazazi wake wawili na ndugu watatu akizungumza na vyombo vya habari

Madiwani wamesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kutambua mchango mkubwa alioutoa marehemu baba yake aliyefahamika kwa jina la Linton Zambi, wakati akiwa mtumishi wa Halmashauri hiyo.

Hivi karibuni kupitia ukurasa wake wa Twitter Waziri wa Afya, Maendeleo Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, alieleza kuguswa na tukio la kupoteza wazazi wawili, na ndugu zake watatu lililomkuta mwanafunzi Anna Zambi na kuahidi kama Waziri wenye dhamana atamsaidia mtoto kwa njia yeyote.

Waziri Ummy aliandika kuwa "hili jambo ni kubwa mno kwa mtoto Anna Zambi, inaumiza sana ninamuombea kwa Mungu ampe nguvu na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu."

"Kama mzazi na Waziri mwenye dhamana ya Ustawi na Maendeleo ya Watoto nami nitamfikia Anna kwa ajili ya kumfariji na 'support' nyingine." ameongeza Waziri Ummy

Wazazi walikuwa wakifahamika kwa majina ya Lingston Zambi na Winifrida Lyimo na wadogo zake watatu, Lulu, Andrew na Grace walikufa katika ajali hiyo baada ya gari walilokuwa wamepanda kusombwa na maji kutokana na mvua kubwa iliyonyesha wilayani Handeni mkoani Tanga.