Ijumaa , 23rd Feb , 2018

Rais Dkt. John Magufuli ametoa wito kwa nchi ya Sudani Kusini kumaliza tofauti zake walizokuwa nazo ili wananchi wa nchi hiyo waweze kujikita katika kulijenga taifa hilo.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Sudani Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit katika hoteli ya Munyonyo Mjini Kampala leo asubuhi tarehe 23 Februari, 2018 kabla ya kuanza kwa vikao vya mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

"Nimemhakikishia  Rais Salva Kiir kuwa Tanzania ipo pamoja na Sudani Kusini na tunapenda tofauti zinazosababisha matatizo nchini mwake ziishe, sisi Tanzania tupo tayari kufanya biashara na Sudani Kusini, hata chakula kama wanahitaji tutawauzia", amesema Rais Magufuli.

Kwa upande wake Rais Salva Kiir Mayardit amesema Tanzania na Sudani Kusini zina uhusiano wa kihistoria tangu enzi ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na kwamba japo kuna vita nchini mwake Rais Magufuli amemhakikishia kuwa uhusiano na ushirikiano huo utaendelezwa na kukuzwa zaidi.