Jumatano , 19th Feb , 2020

Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es Salaam, Janeth Mtega, ameutaka upande wa mashtaka kueleza ni wapi umefikia upelelezi wa kesi inayomkabili Ofisa wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC), Tito Magoti na mwenzake Theodory Giyan.

Theodory Giyan na Tito Magoti wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hakimu Mtega amehoji suala hilo leo Februari 19, 2020, wakati kesi hiyo ilipofikishwa mahakamni hapo kwa ajili ya kutajwa na kusema kuwa upande wa mashtka unapaswa kuheshimu amri ya Mahakama sio kila mara wadai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.

Wakili Mtega ameeleza kuwa mnamo Februari 5, 2020, Mahakama hiyo iliutaka upande wa mashtaka wakirudi tena waeleze upelelezi wa shauri hilo ulipofikiwa kwa lengo la kujua unakwenda mbele au umesimama.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 04, 2020.

Tito na mwenzake Theodory wanakabiliwa na mashtka matatu, ikiwemo kushiriki genge la uhalifu, kumiliki programu ya kompyuta pamoja na utakatishaji wa fedha shilingi Milioni 17, makosa ambayo wanadaiwa kuyatenda kati ya Februari 1 na Disemba 17, 2019 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.