Jumatatu , 8th Jul , 2019

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema mfumuko wa bei wa Taifa Kwa mwaka ulioishia mwezi juni, umeongezeka hadi asilimia 3.7 kutoka asilimia 3.5 kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2019.

Taarifa hiyo imetolewa leo Julai 8, na Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Daniel Masolwa, amesema ongezeko hilo linamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidha na huduma kwa mwaka ulioishia juni imeongezeka  ikilinganishwa na Mei. 

''Ongezeko la mfumuko wa bei Kwa mwaka ulioisha mwezi Juni, kumechangiwa na kuongezeka kwa bei za bidhaa za vyakula, na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi cha mwaka ulioisha mwezi Juni, 2019 ikilinganishwa na Juni 2018.

Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko huo, ni unga wa mahindi asilimia 3.6, ngano asilimia 4.4, mtama asilimia 4.9, samaki wabichi asilimia 27.3," 

Ambapo kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia ongezeko hilo, ni pamoja na dizeli kwa asilimia 11.4, petroli asilimia 4.9, nyumba za kulala wageni asilimia 5.8 na vitabu vya shule vikiwa ni asilimia 2.4.

Aidha Masolwa amefafanua hali ya mfumuko wa bei Kwa Nchi za Afrika Mashariki, ambapo Uganda mfumuko wa bei ulioishia Juni mwaka huu, ulikua asilimia 3.4 kutoka asilimia 3.3, huku Kenya ongezeko likifikia asilimia 5.70 kutoka asilimia 5.49.