Jumamosi , 24th Mar , 2018

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametembelea mradi wa ujenzi wa jengo la tatu la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) na kwamba ameridhishwa na maendeleo yake.

Mradi wa ujenzi wa jengo hilo umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika Juni 2019 na utakuwa na uwezo wa kuegesha ndege kubwa 24 kwa wakati mmoja, pamoja na kuhudumia abiria milioni sita kwa mwaka.

Akiukagua mradi huo Waziri Mkuu amefarijika na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo pamoja na kukuta Watanzania wengi wakishiriki katika kazi za ujenzi.

Amesema mbali na ujenzi wa jengo hilo, pia Serikali  inaendelea kuvikarabati viwanja mbalimbali vya ndege nchini kikiwemo cha Musoma, Iringa, Kilwa Masoko, Lake Manyara, Lindi, Moshi, Njombe, Tanga, Simiyu, Singida na Songea ili kuboresha huduma za usafiri wa anga nchini.