Jumatatu , 18th Feb , 2019

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali haitomvumilia mtu yeyote atakayebainika kuhujumu mkakati wake wa kulifufua zao la michikichi nchini.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Amesema anataka kuona wakulima wa zao hilo wakinufaika kama wengine wa mazao makuu ya biashara, hivyo haitomfumbia macho mtu atakayezembea.

Akikagua shamba la michikichi la kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Bulombora Majaliwa amesema kwamba Serikali inataka kuona wakulima wa zao hilo wakinufaika kama ilivyokuwa kwa wakulima wa korosho, chai, kahawa, pamba na tumbaku.

"Serikali imeamua kulifufua zao hili kwa lengo la kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kupikia, kwani inatumia fedha nyingi kuagiza nje ya nchi", amesema Majaliwa.

Pamoja na hayo Waziri Mkuu amewaagiza viongozi mkoani Kigoma kwamba suala la kilimo cha michikichi liwe ajenda ya kudumu kwenye vikao vyao huku akiitaka Wizara ya Kilimo ianzishe shamba darasa la zao la michikichi ili wananchi waweze kujifunza mbinu bora za kulima zao hilo.