Jumamosi , 9th Nov , 2019

Hadi kufikia leo Novemba 9, 2019, jumla ya vyama vitatu vya upinzani vimeamua kujitoa kushiriki katika kinyang'anyiro cha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kile walichokieleza kuwa asilimia kubwa ya wagombea wake majina yao yameenguliwa.

Waziri wa TAMISEMI, mhe. Selemani Jafo

Vyama hivyo ni CHADEMA, ACT - Wazalendo na CHAUMA, ambacho kimejitoa leo, baada ya Chadema kujitoa Novemba 7 na ACT - Wazalendo kilichojitoa siku ya jana ya Novemba 8.

Waziri wa TAMISEMI, Selemani Jafo ameviambia vyama hivyo kuwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa hata kama chama husika kimegoma kushiriki, lazima jina la mgombea lililoteuliwa kushiriki litabandikwa kwenye karatasi ya uchaguzi.

"Uchaguzi utaendelea kama kawaida na kile chama kinachotafsiri demokrasia kinachoitaka, huwezi kulazimisha chama kufanya demokrasia ile unayoitaka wewe. Kwa vyama vilivyojitoa ni uhuru wao kidemokrasia, nivishukuru vyama 11 vilivyosema vitashiriki kwasababu ni muda wao wa kujimwambafai.", amesema Jafo.

"Kwa mujibu wa kanuni, mtu akishateuliwa jina linabaki kwenye karatasi ya uchaguzi hata kama kajiengua mwenyewe", ameongeza Waziri Jafo.

Aidha Waziri Jafo amesema kuwa zaidi ya rufaa 13,500, zimewasilishwa na vyama vya siasa kwenye Kamati za Rufaa za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.