Makamu wa Rais ashangaa wanaohoji ulinzi wa Rais

Jumamosi , 13th Apr , 2019

Makamu wa Rais, mama Samia Suluhu Hassan amewashangaa wale wanaohoji juu ya usalama wa Rais badala ya kuhoji maendeleo yanayoonekana.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan

Ameyasema hayo katika ufunguzi wa mji wa kiserikali katika eneo la Mtumba, nje kidogo ya  Jijini Dodoma pamoja na ofisi za Rais.

Mama Samia amesema, "asubuhi ya leo nilikuwa nasikiliza uchambuzi wa magazeti, kuna mtu anahoji ulinzi wa Rais. Nikasema anahoji ulinzi wa Rais anataka kufanyaje, lakini kabla ya kuhoji ulinzi wa Rais tulidhani atahoji maendeleo yanayoendelea".

"Hii inaonesha kwamba jamaa zetu hawa, kwa vitendo na mambo unayoyaonesha yanawafanya wengine kufilisika, kufilisika kwa mawazo na kufilisika na nini wazungumze katika nchi yetu na ndiyo maana sasa wanelekea kuhoji vitu visivyohitaji kuhojiwa", ameongeza mama Samia.

Tukio hilo la uzinduzi wa mji wa serikali jijini Dodoma limefanywa na Rais John Magufuli, ikiwa ni kuashiria kuwa sasa ni rasmi azma ya serikali kuhamia Makao Makuu Dodoma imekamilika.