Jumapili , 17th Mar , 2019

Serikali imetangaza kutoa ajira 500 kwa walimu watakaopangwa kwenye shule ili kusaidia wanafunzi wenye ulemavu.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu

Akizungumza katika Sherehe za ugawaji tuzo za I CAN zilizoandaliwa na Taasisi ya Dk Reginald Mengi inayoshughulika na watu wenye ulemavu, Makamu wa Rais, Mh. Samia Suluhu amesema kwamba jambo hilo linakuja kutokana na serikali kutilia mkazo kwenye suala la elimu.

"Serikali yenu tumeweka mkazo katika suala la elimu, tunategemea kuajiri walimu 500 waliofundishwa kufundisha watu wenye ulemavu, tutawagawa katika shule tofauti ili waweze kuwasaidia vijana wenye ulemavu," amesema Samia Suluhu.

Mbali na hayo Makamu wa rais, amesema kuwa ni wajibu wa serikali kujenga mifumo wezeshi kwa walemavu kwa kuwa hakuna ajuaye kesho yake atakuwa katika mazingira gani.

Akitoa simulizi Makamu wa Rais anasema kipindi alipokuwa ndiyo kwanza anaanza kazi miaka ya 70 , bosi wake aliyempokea kazini leo hii ndiye Mwenyekiti wa Walemavu huko Zanzibar baada ya kupata ajali.

"Tukikumbuka kuwa sote ni walemavu watarajiwa hakuna mwenye hakika, wanasema kabla hujafa hujaumbwa, sote ni watarajiwa ni jukumu letu sote kujenga mifumo wezeshi, kwasababu yoyote yule anaweza kuingia muda wowote ule", amesisitiza.