Jumapili , 13th Oct , 2019

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda amesema kuwa siku ya kesho maduka yote katika jiji la Dar es salaam yatafunguliwa kuanzia saa 5 asubuhi ili kupisha wananchi kujiandikisha kwenye daftari la mpifa kura kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na kuenzi miaka 20 ya kifo cha

Mwalimu Julius Nyerere.

Mhe. Paul Makonda ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumzia juu ya zoezi la uandikishaji wa wananchi kuelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na kuenzi kifo cha Baba wa Taifa.

Makonda amesema, "kesho Okt 14 ni kumbukizi ya miaka 20 tangu Baba wa Taifa atangulie mbele za haki, kwakuwa kesho ni siku ya mwisho ya kujiandikisha katika daftari la mpiga kura kuwapata Viongozi wa Serikali za Mitaa, kama Mkuu wa Mkoa wa DSM kwa kukuza demokrasia ndani ya Mkoa wetu naelekeza maduka yote yafunguliwe kuanzia saa 5 asubuhi hapa DSM kwakuwa hii ni sehemu ya kumuenzi Baba wa Taifa", amesema Makonda.

"Hii ni katika kuhakikisha wote tunajiandikisha ili kupata haki ya kupiga kura maana Baba wa Taifa aliwapa nafasi kubwa Viongozi hawa", ameongeza.

Kesho Oktoba 14, 2019 ni kumbukumbu ya kifo cha miaka 20 cha Mwalimu Julius Nyerere ambaye alifariki dunia Oktoba 14, 1994 akiwa katika matibabu nchini Uingereza. Pia kesho ni mwisho wa kujiandikisha kwa wananchi kwenye daftari la mpiga kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.