Jumanne , 21st Jan , 2020

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amepokea msaada wa ndoo 500 za rangi kutoka Billion Paints kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa wanafunzi zaidi ya 5,000, walioshindwa kujiunga na kidato cha kwanza kutokana na uhaba wa madarasa.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Akizungumza leo Januari 21, 2020, Makonda amekishukuru kiwanda hicho kwa kuamua kuunga mkono juhudi za Serikali, katika uboreshaji wa sekta ya elimu nchini.

"Mchango huu ni muhimu kwa sababu, Rais wetu anatoa elimu bure na kwenye Mkoa wetu takribani watoto 5,970 katika wilaya moja tu ya Temeke, walikosa madarasa na sasa tupo kwenye ujenzi wa madarasa 381, hivyo tuwashukuru wazawa kwa kuitikia mwito wa elimu, ndoo 500 zitakuwa ni mchango mkubwa sana ambao hauwezi kusahaulika" amesema Makonda.

Waziri wa TAMISEMI Seleman Jafo, aliwaagiza Wakuu wa Mikoa wote nchini kuhakikisha hadi kufikia Februari 28, 2020, wahakikishe wamekamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa ili ifikapo Machi 1, watoto waliokosa masomo kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa, waanze masomo yao.