Alhamisi , 19th Apr , 2018

Malkia Elizabeth wa Uingereza amemtaja mtoto wake wa kiume 'Prince Charles' kuwa huenda akawa mkuu wa jumuiya ya madola kwa miaka ijayo baada ya yeye kuachia ngazi.

Malkia Elizabeth ametoa kauli hiyo leo alipokuwa kwenye mkutano wa nchi za Jumuiya ya Madola (commonwealth) uliofanyika nchini Uingereza, ambapo Tanzania pia imehudhuria.

Akisoma hotuba yake kama mkuu wa Jumuiya hiyo Malkia Elizabeth amesema “ni matumaini yangu kwamba Jumuiya ya Madola itaendelea kutoa utulivu kwa kizazi kijacho, na kuamua kuwa siku moja Mwana Mfalme wa Wales ataendelea kubeba kazi muhimu iliyoanzishwa na baba yangu mwaka 1949”.

Kwa kauli hiyo ya Malkia Elizabeth, ulimwengu unaamini kuwa mtoto wake wa kwanza wa kiume Charles, ndiye atakuwa mrithi wa kuongoza jumuiya hiyo kubwa duniani, ambayo ina nchi wanachama takriban 53.

Kwenye mkutano huo Tanzania imewasilishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, huko jijini London nchini Uingereza.