Mama aua watoto wake sita kwa upanga

Jumatatu , 15th Apr , 2019

Mama mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Nana Maganga mkazi wa Kijiji cha Luzuko Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, anatuhumiwa kuwauwa watoto wake sita kwa kwa mapanga, huku naye akiuawa na wananchi wenye hasira.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley, amesema mauaji ya watoto hao yalitokea jana Aprili 14, 2019, ambapo inadaiwa mama huyo alikuwa mgonjwa wa akili, na watoto watano kati ya sita waliouawa ni aliowazaa mwenyewe na mwingine mmoja ni wa kaka yake.

Kamanda Nley amesema baada ya kufanya mauaji hayo wananchi walisikia kelele na kulazimika kuizunguka nyumba hiyo na kufanikiwa kumdhibiti mama huyo kwa kumfunga kamba mikononi na baada ya muda alifariki dunia kwa kile kinachodaiwa ni kipigo kutoka kwa wananchi wenye hasira.

Aidha kupitia tukio hilo watu watano wanashikiliwa kwa kusababisha mauaji ya Mama huyo akiwemo Mganga mmoja wa Kienyeji.