Ijumaa , 23rd Mar , 2018

Aliyekuwa Spika wa Bunge Bi. Anna Makinda ameshauri madiwani wanawake kuhakikisha wanajenga hoja zitakazozifanya halmashauri zao kuwatambua wanawake walio nje ya mifumo ya kifedha ili kuwasaidia kupata mikopo inayotolewa kupitia fungu la uwezeshaji.

Mama Makinda ameto wito huo jijini Dar es Salaam leo na kufafanua kuwa asilimia kumi ya fedha zinazotengwa na kila halmashauri nchini zimelenga kuwainua kiuchumi wanawake hao ambapo hawapo kwenye vikundi kama VICOBA, SACCOS na aina nyingine za makundi ya kijasiriamali.

Akifafanua hoja hiyo, Spika huyo mstaafu ameshauri njia nyingine ambayo madiwani wanawake wanaweza kuitumia kuwa ni kupitia mabaraza ya madiwani ambako wanatakiwa kutoa ushauri wa kuongeza vyanzo vya mapato.

Amesema ili hiyo asilimia kumi inayotengwa kuinua wananchi kiuchumi iwe ya kutosha na kuwafikia wahitaji wengi zaidi wanahitajika kupaza sauti zao.