Ijumaa , 23rd Mar , 2018

Makamu wa Rais wa Tanzania na  Samia Suluhu Hassan amewata wanachama wa CCM Kisiwani Pemba kuwa kitu kimoja kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2020 ili waweze kunyakua majimbo mengi.

Mh. Samia ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wanachama wa chama hicho Jimbo la Ole, Wilaya ya Chakechake baada ya kuweka jiwe la msingi la tawi la CCM, amesema kitendo cha wanachama wa chama hicho kutokuwa na furaha katika kisiwa hicho ni miongoni mwa sababu zinazowafanya washindwe kujipanga na hatimaye chama cha upinzani kushinda katika majimbo yote.

Amesema anajua ndani ya CCM wapo baadhi ya watu hawana hamasa, jambo ambalo linaonyesha ni kama chama hicho hakipo kwenye jimbo hilo na maeneo mengine ya Pemba na kusahau kuwa CCM ndicho chama pekee kinachoongoza Serikali.

Mama Samia amebainisha kuwa, kuna baadhi ya wanachama wamekuwa wakila kiapo cha kukilinda chama, lakini kinyume chake hushindwa kutekeleza majukumu yao kutokana na kile alichokiita kuwa ni woga usiokuwa na tija. “Ni lazima vijana wa CCM mjenge ujasiri na uthubutu"

Pamoja na hayo, amewataka wana CCM kisiwani humo kuacha tabia ya kuwatenga wanachama wa vyama vya upinzani, badala yake wawashawishi ili wajiunge kwenye chama chao alichokitaja kuwa ni bora zaidi na chenye kujali masilahi ya wananchi wote.