Ijumaa , 14th Sep , 2018

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya  Dar es salaam, Lazaro Mambosasa, amevitahadharisha vikundi vya vijana ambavyo vinatumika kisiasa kutaka kuvunja amani kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge katika jimbo la Ukonga kwa kisingizio cha kulinda kura.

Kamanda Lazaro Mambosasa

Akiongea leo kwenye mkutano na wanahabari, Mambosasa amesema, jeshi lake limejipanga vyema kuhakikisha uchaguzi huo unaanza na kumalizika salama huku mshindi akitarajiwa kupatikana kwa ushindi wa kura na si vinginevyo.

''Kuna vitendo vimekuwa vikijitokeza kwenye chaguzi, ambapo vikundi vya vijana vinajiita walinda kura, kitu ambacho ni kinyume na sheria hivyo watakaofanya hivyo kwenye uchaguzi wa Ukonga wataishia kwenye mikono ya dola'', amesema.

Mambosasa amesema watahakikisha usalama wa zoezi zima kuanzia kusambazwa kwa vifaa vya kupigia kura katika vituo vyote hadi kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo unaofanyika Jumapili Septemba 16, 2018.

Katika uchaguzi huo wagombea wa vyama vya CHADEMA na CCM, wanachuana vikali ambapo CCM inawakilishwa na Mwita Waitara huku CHADEMA wakiwakilishwa na Asia Msangi.

Mbali na hilo Mambosasa ameibanisha jeshi hilo limefanikiwa kukamata watuhumiwa 8 akiwemo mwanamke mmoja, wanaodaiwa kuendesha vitendo vya uporaji wa Bajaj katika eneo la Mvuti Gongo la mboto jijini Dar es salaam.