Ijumaa , 12th Oct , 2018

Afisa Habari wa Simba, Haji Manara amekamatwa na polisi kutokana na tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’. Manara alikamatwa jana jioni na kuachiwa kabla ya leo asubuhi Oktoba 12, 2018 kukamatwa tena na polisi.

Haji Manara akiwa na Mo Dewji.

Akithibitisha kukamatwa kwa Manara, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema Manara anashikiliwa kutokana na kusambaza taarifa za tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii kwa madai ya kutumwa na familia, jambo ambalo si la kweli.

“Manara tunamshikilia kwa uchunguzi zaidi yeye amekuwa akisambaza taarifa mbalimbali za tukio hili kwenye mitandao ya kijamii kwa madai kuwa ametumwa na familia, lakini sio kweli, hajatumwa na familia hivyo tunamshikilia ”, amesema Kamanda Mambosasa.

Taarifa za kutekwa kwa mfanyabiashara huyo anayekadiriwa kuwa na utajiri wa Sh3.5 trilioni zilianza kusambaa Alhamisi saa 1:00 asubuhi katika mitandao ya kijamii, kabla ya polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam kuthibitisha saa mbili asubuhi.

Mapema jana Manara alinukuliwa akisema taarifa ya Mo kupata matatizo imemshtua kila mmoja na kwamba bado wanaliachia jeshi la polisi kufanya kazi ya kumpata mwekezaji wao. “Wanasimba wawe watulivu wakiliachia jeshi la polisi kufanya kazi yake na kwamba wanaamini MO atapatikana akiwa hai,” alisema Manara.