Jumapili , 6th Oct , 2019

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi, amesema kuwa mataifa makubwa Duniani ikiwemo Marekani, wamekuwa wakiipongeza nchi ya Tanzania kwa kuweza kujisimamia yenyewe kiuchumi, ikiwemo katika ununuaji wa ndege zake.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi

Waziri Kabudi ameyabainisha hayo leo Oktoba 6, 2019, wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, mkoani Rukwa na kwamba utendaji wake wa kazi umewarahisishia wao katika kuifanyakazi ya Diplomasia katika mataifa mbalimbali Duniani.

''Mh Rais nimetoka Marekani, moja ya mambo ambayo sitaki kuyasema ni nani aliniambia,alisema tunawashukuru watanzania kwa kununua ndege zetu tena bila mikopo, imetupa heshima hatuendi kuomba, hatuendi kukopa tunanunua Cash, huko nje hatutetereki, hatuendi kama wanyonge,tunaenda kwa nguvu kwa sababu ya mambo yaliyofanyika na nchi hii'', amesema Profesa Kabudi.

Aidha Profesa Kabudi ameongeza kuwa licha ya kuwepo kwa watu wanaoenda katika mataifa mbalimba kwa nia ya kuichafua nchi, lakini yeye kama mwanadiplomasia amekuwa akitolea ufafanuzi na kusema kuwa Tanzania imekuwa ikiongoza kwa haki katika mambo mbalimbali.

''Kwasababu watu Mh Rais huko Duniani, wamekosa ya kusema ndio maana, wanakwenda katika mambo yasiyokuwa ya msingi na hata wale wapotoshaji wa ukweli wa nchi hii, huko nje tumekuwa tukienda kufafanua ukweli na tunapata nguvu hiyo kwa sababu ya nguvu kubwa uliyoifanya'' amesema Profesa Kabudi.