Jumanne , 19th Mar , 2019

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt Vincent Mashinji amezngumzia sababu za Maalim Seif Sharif Hamad kutojiunga chama hicho, licha ya wao kuwa wa kwanza kuongea naye.

Dkt Vincent Mashinji ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na www.eatv.tv iliyotaka kufahamu kuhusiana na tukio la Maalim Seif kujiunga na ACT - Wazalendo muda mfupi baada ya Mahakama kumtangaza Prof. Ibrahim Lipumba kuwa mshindi wa kesi ya uhalali wa uenyekiti wake ndani ya chama hicho.

"Mimi nadhani kueleza kilichotokea mpaka hakujiunga kwetu na akaenda ACT - Wazalendo yeye mwenyewe ndiyo anaweza kulieleza lakini ninachoweza kusema, Katiba inatungwa na chama wala sio Katibu kama alisoma katiba mbalimbali akaona ya kwetu haimvutii basi hivyo ndiyo tulivyo." amesema Maalim.

Wakati akitangaza uamuzi wa kujiunga na ACT - Wazalendo Maalim Seif amesema alizungumza na vyama karibua 10 vya upinzani lakini akagundua masharti ya ACT - Wazalendo ndiyo yaliyokuwa ya unafuu zaidi.

Mara baada ya Maalim Seif kutangaza kujiunga na ACT - Wazalendo Katibu Mkuu huyo wa CHADEMA alimpongeza kwa uamuzi wake huo na kusema ni faida kubwa sana kwao.

Mapema jana Machi 18, 2019, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es salaam ilitangaza kutambua uhalali wa mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa Profesa Ibrahim Lipumba.

Kufuatia maamuzi hayo ya Mahakama, majira ya saa nane mchana Machi 18, 2019, Maalim Seif alitangaza uamuzi wa kuhamia Chama cha ACT- Wazalendo kwa kile alichokidai amesoma katiba za vyama vingine na kubaini masharti ya chama hicho ni nafuu zaidi.