Jumamosi , 12th Sep , 2020

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa hospitali binafsi na za Serikali kujenga wodi maalumu zilizojitenga kwa ajili ya ugonjwa wa saratani ili kuweza kutoa huduma zenye uhakika katika uchunguzi na tiba zake.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Majaliwa ameyasema hayo wakati akihutubia katika hitimisho la mbio za NMB BIMA Marathon zilizofanyika leo Septemba 12,2020 katika eneo la Mlimani city Jijini Dar es Salaam ambazo zinalengo la kusaidia watoto wenye saratani katika hospitali ya Taifa Muhimbili na kuwataka wadau kushirikiana na serikali ili kuboresha huduma za afya.

‘’Nitoe wito kwa hospitali zote za serikali na binafsi kujenga wodi maalumu kwenye maeneo yao zilizojitenga ili kuweza kutoa huduma hii kwa uhakika kuanzia uchunguzi hadi tiba yake’’, amesema Majaliwa.

‘’Milioni 100 zimekusanywa zitakazoweza kusaidia watoto wenye saratani waliopo hospitali ya Muhimbili, niwapongeze wote mlioshiriki katika mbio hizi, naelewa bado kuna makundi ambayo yanahitaji misaada yetu’’, ameongeza.

Aidha Majaliwa amewapongeza wote walioshiriki katika mbio hizo za hisani na kuwataka kutoishia hapo kwani kuna kundi kubwa ambalo bado linahitaji msaada.