Maua Sama awaibua BoT, watoa tamko

Jumatano , 19th Sep , 2018

Benki kuu ya Tanzania (BOT) imetoa onyo kwa wananchi kuheshimu fedha ya Tanzania kwakuwa ni moja ya alama ya taifa na kuonya kwamba kudhihaki na kukejeli noti na sarafu ni kosa la jinai.

Msanii wa muziki wa bongo fleva Maua Sama.

Tamko hilo limetolewa kufuatia matukio ya hivi karibuni ya baadhi ya wananchi kuonekana wakifanya dhihaka noti za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzirusha ovyo na kuzikanyaga. Hali iliyopelekea wengine kuchukuliwa hatua za kukamatwa na Jeshi la Polisi akiwemo msanii wa muziki wa kizazi kipya Maua Sama baada ya kuweka 'video' kwenye mtandao wake wa kijamii ikionyesha wakichezea noti ya shilingi elfu kumi huku wakiimba wimbo wake mpya unaokwenda kwa jina la 'Iokote'.

Taarifa ya BoT kwa vyombo vya habari ambayo wameitoa, inasema utunzaji mzuri wa fedha utapunguza uwezekano wa fedha hizo kuchakaa mapema na kupunguza gharama za uchapishaji.

"Kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006, kifungu cha 26, BoT ndiyo taasisi pekee yenye mamlaka ya kutoa noti na sarafu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," imesema taarifa hiyo.

Taarifa imesisitiza kuwa, “Benki Kuu pekee ndiyo yenye mamlaka ya kuharibu noti na sarafu (kifungu cha 28 kikisomwa pamoja na kifungu cha 30 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006”.

Msanii Maua Sama ambaye taarifa ya kukamatwa kwake ilitolewa Kamanda wa Polisi mkoa wa Dar es salaam, Lazaro Mambosasa hadi sasa bado anashikiliwa polisi katika kituo cha kati jijini Dar es salaam toka siku ya Jumapili na hadi sasa taarifa zinasema bado hawajafikishwa mahakamani uchunguzi zaidi ukiendelea.

Soma zaidi hapo chini taarifa ya BoT.