Jumatano , 19th Sep , 2018

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetangaza kujiondoa rasmi kushiriki chaguzi ndogo zote zilizotangazwa kufanyika hivi karibuni na chaguzi zozote zitakazofuata zinazosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa madai kwamba tume hiyo inafanya kazi ya Chama Cha Mapinduzi.

Mwenyekiti wa CHADEMA taifa, Freeman Mbowe.

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 19, na mwenyekiti wa Chadema taifa, Freeman Mbowe ameituhumu NEC akidai inafanya kazi ya kuhakikisha chama tawala chini ya kinashinda kwa kulazimisha matokeo hivyo hawatashiriki katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Liwale na kata 37 kwa kile alichodai kuwa, chama kinapitia maumivu mazingira magumu ya kisiasa.

Ukonga kulikuwa na vituo feki 16 vyenye wapiga kura zaidi ya 7,000 na viliandaliwa mahususi kwa ajili ya kuongeza kura za CCM. Tulipeleka malalamiko yetu NEC na kwa msimamizi wa Uchaguzi, hakuna kilichofayika.

Mbowe ameongeza kuwa “Upole na ukimya wa vyama vya upinzani hauashirii uoga hata kidogo, yale mawazo ya wenzetu wa Chama Cha Mapinduzi kuamini wana dola na ndio wenye nguvu ni kujidanganya, hakuna jeshi linaloweza kuwa na nguvu kuwazidi raia wa Tanzania.

Hayo yanajiri kufuatia kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa Septemba 16, katika majimbo ya Monduli na Ukonga ambayo CCM ilishinda majimbo yote na CHADEMA kupoteza majimbo hayo ambayo mwanzo yalikuwa yakishikiliwa na chama hicho baada ya waliokuwa wabunge wake kujiuzulu na kujiunga na CCM.