Alhamisi , 18th Apr , 2019

Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Upendo Peneza amesema ni aibu kwa Chama cha Mapinduzi kuwa na Katibu Mwenezi kama Humphrey Polepole ambaye anadhalilisha wanawake.

Polepole

Peneza ameyasema hayo wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2019/20.

Peneza amesema kwamba Mwenezi Humphery Polepole, amewadhalilisha wabunge wa viti maalumu wanaotokana na chama chake kuwa wamepata nafasi hizo baada ya kufanya ngono na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Amesema kuwa wabunge wa viti maalumu wapo kwa mujibu wa Katiba lakini kuna kitu kibaya kilianza kutokea ndani ya Bunge na kwamba, viongozi wa Bunge wanapokaa kuendesha Bunge wamekuwa wakikemea tabia hiyo aliyoiita ni ya kipuuzi.

Amesema ifike wakati watu watambue huo ni udhalilishaji ambao hauruhusiwi na sheria za Tanzania na kwamba Polepole amefanya kazi katika taasisi za Serikali muda mrefu.

“Sasa kama hata hatambui haki za kikatiba ni aibu kwa Chama cha Mapinduzi kuwa na mwenezi anayedhalilisha wanawake… lakini ifike mahali nafasi walizonazo na vyeo walivyonavyo viheshimiwe. Ni aibu kwa kiongozi wa nchi hii kusimama na kusema kwamba mafanikio ya mwanamke ya kisiasa yanatokana na shughuli za kingono, tunawajengea watoto wetu fikra mbaya ndani ya kichwa chao", amesema Peneza.

Ameongeza kuwa, "tunawajengea watoto wetu fikra mbaya, hakuna tena jitihada ila jibu pekee waende wakafanye ngono watapata nafasi".