Jumatatu , 22nd Apr , 2019

Mbunge wa Kyadondo Mashariki Robert Kyagulanyi  'Bobi Wine' amekamatwa baada ya yeye na wafuasi wake kugombana na maafisa wa polisi kufuatia hatua ya mamlaka kufutilia mbali tamasha lake la muziki la siku kuu ya pasaka.

Mbunge wa Kyadondo Mashariki Robert Kyagulanyi  'Bobi Wine'.

Kulingana na gazeti la Daily Monitor nchini Uganda Mbunge wa Makindye Magharibi Allan Ssewanyana alizirai na ikalazimika wafuasi wake kumbeba hadi katika gari moja ambalo lilikuwa likimsubiri.

Hali ya wasiwasi ilitanda baada ya maafisa wa polisi kuuzuia msafara uliokuwa ukiongozwa na mbunge huyo katika tamasha lake la One Love huko Busabala.

Wawili hao walikamatwa mapema siku ya Jumatatu na kuzuiliwa katika gari moja la maafisa wa polisi kabla gari hilo kuondoka nao.

Kukamatwa kwa Bobi Wine kunajiri baada ya rais Yoweri Museveni kusema kuwa hatokubali matamasha ya muziki uliojaa siasa na kuonya kwamba katika siku za usoni hakuna mtu atakayefidiwa kwa matamasha ambayo yamefutiliwa mbali kutokana na siasa.

Bobi Wine alikamatwa na kuingizwa katika gari la polisi na kupelekwa eneo lisilojulikana.

Awali polisi walitumia nguvu kulifungua gari ambalo mbunge huyo kabla ya kuvunja vioo vyake na kumtoa nje.