Alhamisi , 18th Apr , 2019

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku (Musukuma) ameitaka Wizara ya Katiba na Sheria kufanya marekebisho ya baadhi ya sheria zinazoonekana hazina manufaa kwa mazingira ya sasa.

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku (Musukuma)

Musukuma ametoa kauli hiyo katika vikao vya Bunge kwenye mjadala wa Wizara ya Katiba na Sheria ambapo kupitia Waziri wa Katiba na Sheria, Agustino Mahiga aliwasilisha makadirio ya bajeti yake.

"Niseme tu kiukweli ni vizuri mkaangalia mkarekebisha sheria, hasa kwenye makosa madogodogo ambayo yamepelekea magereza mengi kujaa mahabusu ambayo kwa kweli mengine yanastahili makofi tu mtu akaenda nyumbani", amesema.

Musukuma ameongeza kuwa, "nashauri sana hizi sheria zilizotungwa tukiwa milioni 20, leo tuko milioni 55 mtu anawekwa wiki 2 kwa kesi ya kuiba kuku, ni vitu ambavyo tufikirie adhabu ili kupunguza mrundikano wa mahabusu kule ndani."

"Nilisoma kwenye kitabu cha Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusiana na uteuzi wa Majaji, inampa mamlaka Rais kuteua na anakuwa jopo la kumshauri ninawataka tu wenzangu wamuachie Rais akafanya majukumu yake." amemalizia Musukuma.

Kwa sasa Bunge linaendelea jijini Dodoma ambapo Wabunge wanakaa kama kamati kwa ajili ya kujadili namna Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara mbalimbali.