Jumapili , 12th Aug , 2018

Jeshi la Polisi mkoani Arusha limesema limefungua jalada la uchunguzi la tukio la vurugu katika uchaguzi mdogo wa marudio kata ya Kaloleni jijini Arusha baada ya watu wawili kudaiwa kuchomwa visu na kikundi cha vijana wa 'Green guard' kutoka CCM. 

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Ramadhani Ng'azi

Akizungumza na www.eatv.tv Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Ramadhani Ng'azi amesema walipigiwa simu na Mbunge wa Arusha wa Mjini (CHADEMA), Godbless Lema kuwa mgombea wao Boniface Kimario amevamiwa na kuamuru askari waliokuwa karibu na maeno hayo kuenda kutuliza hali ya usalama.

"Asubuhi kulitokea ushabiki wa kisiasa kati ya makundi mawili ambayo ni ndio sasa hivi tunachunguza, na ushabiki huo ndio ulisababisha huyo mgombea wa CHADEMA kupigana na watu wengine. Kutokana na maelezo yake amesema akiwaona hao watu anawatambua hivyo tunamsubiri amalize kutibiwa ili aje atuambie ni wakina nani hasa. Lakini yeye hakuchomwa kisu", amesema Kamanda Ng'azi.

Pamoja na hayo, Kamanda Ng'azi ameendelea kwa kusema "isipokuwa kuna mwanachama mmoja wa CCM alijeruhiwa na kitu chenye ncha kali juu ya kiwiko chake cha mkono wake wa kulia. Tumeshamkamata mtuhumiwa mmoja ambaye amemjeruhi mwanachama wa CCM"

Mbali na hilo, Kamanda Ng'azi amesema hali ya uchaguzi inaendelea vizuri katika mkoani mzima wa Arusha hadi hivi sasa ambao una jumla ya kata tatu ambazo ni Kaloleni, Daraja Mbili pamoja na Osinyayo.

Msilikize hapa chini, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Ramadhani Ng'azi akisimuliza zaidi juu ya tukio hilo.