Jumapili , 5th Jan , 2020

Mhubiri Elisha Misiko wa kanisa la Ground for Jesus, lililoko mjini Mombasa nchini Kenya, amemuua mke wake kwa kumchoma na kisu na kisha yeye kujikata koo lake na kufariki papo hapo, wakati wa ibada ya Jumapili ikiendelea kanisani hapo.

Pichani ni kanisa ambalo mauaji hayo yamefanyika.

Tukio hilo limetoa leo Januari 5, 2020, ambapo kwa mujibu wa waumini wa kanisa hilo wamesema kuwa mhubiri huyo alitekeleza unyama huo kwa haraka sana na kwamba juhudi za kuwanusuru wawili hao hazikuzaa matunda.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa eneo la Kisauni, Julius Kiragu, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea majira ya saa 4:00 asubuhi ya leo na kwamba Jeshi la Polisi mjini Mombasa, limekwishaanza kufanya uchunguzi ili kubaini nini chanzo kilichopelekea mume kumuua mkewe na kisha yeye naye kujikata koromeo.

Aidha Kamanda Kiragu amesema kuwa ndani ya mfuko wa suruali wa mhubiri huyo wakati wakiondoa mwili wake na kuupeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti, wamekuta barua yenye kurasa 17, iliyokuwa ikieleza chanzo cha mauaji hayo kuwa ni migogoro ya kifamilia.