Ijumaa , 20th Apr , 2018

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefunguka na kudai kuna ugonjwa umewaingia watanzania wa kupenda kuamini kila kitu kitakachokuwa kinaandikiwa na kuwekwa katika mitandao ya kijamii hata kama sio za kweli.

Dkt. Magufuli amesema hayo leo April 20, 2018 wakati akiwaapisha Majaji, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali na Naibu Mkurugenzi wa Mashitaka, Ikulu jijini Dar es Salaam na kusema kuwa watu wanatumia uhuru wao vibaya na kupotosha watu kuhusu upotevu wa fedha hizo na kuleta taharuki katika nchi. 
 
"Kuna ugonjwa tumeupata sisi watanzania wa kuamini kila kinachoandikwa kwenye mitandao ni cha kweli, sasa sijui huu ugonjwa umetoka wapi lakini ni kwasababu hii mitandao hatui-control sisi. Wako huko wenye mitandao yao ambao wenyewe wako busy na kutengeneza bussiness na hawajali na matatizo mtakayopata na ndio maana mkienda katika nchi kama China sina uhakika kama wana Google na WhatsApp kama tulizonazo sisi ndio maana kila mmoja anapojifikiria ana-post chochote", amesema Dkt. Magufuli. 

Kwa upande mwingine, Rais Magufuli amesema uwepo wa uhuru nchini ndio unasababisha kila mtu ku-post kile anachojisikia katika mitandao ya jamii na kuwaaminisha watu.